Jumatano 1 Julai 2026 - 13:20
Dhamana na Ujumbe wa Shahada ya Imam Shahidi kwa Iran na Ulimwengu wa Kiislamu

Hawza/ Sherehe ya mazishi ya mwili mtukufu wa Imam Shahidi inapaswa kurekodiwa kama tukio la kipekee lisilofungwa na mipaka ya wakati wala mahali. Mkusanyiko wa shakhsia kubwa za ulimwengu wa Kiislamu, alama za kimataifa, vyombo vya habari vyenye ushawishi vya Umma wa Kiislamu, wanazuoni, wasomi, wapiganiaji na watu huru dunianj vitasaidia kuifanya hamasa hii ing'ae katika kiwango cha kimataifa na kufikisha ujumbe mkubwa wa Imam Shahidi kwenye nyoyo za watu katika mabara yote, hususan katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ifuatayo ni matini kamili ya ujumbe muhimu na wa kimkakati wa Ayatullah Alireza A'rafi, Mkuu wa Hawza za Kielimu, kwa mnasaba wa siku za kuuaga, kuusindikiza na mazishi ya kihistoria ya mwili mtukufu wa Shahidi, Hadhrat Ayatullah al-Udhma Imam Khamenei (ra):

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

﴿وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِینَ قُتِلُوا فِی سَبِیلِ اللَّهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْیَاءٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ یُرْزَقُونَ﴾

﴿مِنَ الْمُؤْمِنِینَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَیْهِ فَمِنْهُم مَّن قَضَیٰ نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن یَنتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِیلًا﴾

Ee Umma mkubwa wa Kiislamu, enyi watu huru na waliodhulumiwa duniani, enyi mataifa yaliyoamka na dhamiri zilizo hai katika pembe zote za dunia.

Leo ulimwengu wa Kiislamu, bali hata ubinadamu wote wenye kiu ya uadilifu, umo katika maombolezo ya kuondokewa na kiongozi ambaye hakuwa mali ya mpaka mmoja wala taifa moja, bali alikuwa hazina ya pamoja ya Umma wa Kiislamu na mrithi wa njia ya Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu.

Shahada ya kidhuluma ya kiongozi mwenye hekima, Marjaa Mkuu na nahodha wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hadhrat Ayatullah al-Udhma Imam Khamenei (A'la Allahu Maqamah), si tukio linaloweza kujifunga ndani ya mipaka ya eneo fulani la kijiografia. Tukio hili linapaswa kusomwa kwa kiwango cha mlinganyo wa ulimwengu wa Kiislamu na katika upeo wa mabadiliko makubwa ya ubinadamu. Mtukufu huyo alikuwa mkusanyiko wa fadhila zisizo na idadi na sifa za kipekee, mionekano ya shakhsia yake ya kipekee iling'aa nchini Iran na ulimwenguni, ikabadilisha mlinganyo wa dunia na kuwa sababu ya maendeleo mbalimbali pamoja na utukufu wa Iran na Umma wa Kiislamu.

Imam Shahidi alikuwa kielelezo cha fikra zenye mtazamo wa kidunia, mawazo yake yalivuka mipaka ya kikabila na kitaifa na kuweka msingi wa mjadala wa kimataifa ambao ndani yake maadili ya pamoja ya kibinadamu, heshima ya mwanadamu, uadilifu na kusimama dhidi ya ubeberu vilipata lugha inayowafikia wote. Alielewa kwa kina changamoto na vitisho vya kimataifa na alizungumza kwa lugha inayolingana na zama za ustaarabu, teolojia aliyoiwasilisha ilikuwa teolojia ya kimataifa ya ukombozi; mafundisho yaliyomleta Mwenyezi Mungu katikati ya maisha ya waliodhulumiwa na kuifanya imani kuwa nguvu ya ukombozi wa mataifa. Hadhi yake ya juu ya Marjaiyya pia ilikuwa katika mwelekeo huo huo; Marjaiyya iliyounganisha fiqhi na wajibu wa kihistoria pamoja na dhamana kwa Umma, alikuwa baba wa taifa, roho ya hadithi ya Muqawama, kiongozi wa Umma na roho ya taifa.

Uhalifu wa kutisha uliofanywa na wahalifu wa Marekani na Israel uliosababisha shahada hii, katika fikra nyeusi za waandaaji wake, ulilenga kuipiga harakati hii, taifa hili na dola yake pigo la mauti na kusababisha kuporomoka kwake kwa ghafla. Hapo ndipo moja ya nyanja za ukubwa wa uongozi wake inapodhihirika, kwa miaka mingi alikuwa akiujenga Umma na pia akiijenga dola; aliwaunganisha watu si kwa nafsi yake, bali kwa Mwenyezi Mungu, misingi na malengo makubwa yenye kutoa nguvu na uhai, viongozi wanaowekeza kwenye mvuto wao binafsi, mvuto huo unapoporomoka taratibu na dola zao pia huporomoka.

Lakini mfano wa uongozi wa Imam Shahidi ulikuwa wa namna ambayo, licha ya makadirio yote ya kimkakati ya maadui kuhusu machafuko na kuporomoka, kila jambo liliendelea kwa namna ya kimiujiza katika njia ya uthabiti na mshikamano. Huu pia ni ushahidi mwingine wa ukweli na undani wa madhehebu haya ambayo yanawaunganisha watu na Mwenyezi Mungu, si na watu binafsi.

Ee Umma uliokomaa! Hisia ya kulipiza kisasi kwa damu hii takatifu inapaswa kubaki hai na endelevu ndani ya nyoyo; si kama mwali unaowaka kwa muda mfupi, bali kama azma ya kudumu ya kuifuata njia ileile ambayo yeye aliinyweshea kwa damu yake. Damu ya mashahidi ni taa ya kuongoza njia, na uaminifu kwa malengo yao ndiyo maana halisi ya kulipiza kisasi kwa ajili yao. Kulipiza kisasi kwa Imam Shahidi si mapambano ya kihisia wala ya msisimko, bali ni mwendelezo wa kupambana na dhulma na ubeberu katika mfumo mpya, na ni mojawapo ya majukumu makuu na ya msingi ya Muqawama.

Shahada yake ina dhamana na ujumbe ulio wazi kwa viwango mbalimbali vya ulimwengu wa Kiislamu na Iran.

Ujumbe wa kwanza ni kwamba; shahada ni mtaji wa Umma, si hasara yake; na ni sababu ya fedheha na maangamizi kwa adui, si mafanikio kwake. Maadui walidhani kwamba; kwa kumuua kwa njia ya kigaidi kiongozi msomi na mwenye hekima wa Iran, wangevunja azma ya taifa. Lakini Sunna ya Mwenyezi Mungu ni kwamba damu safi ya mashahidi huifanya mizizi ya imani kuwa yenye kina zaidi, huimarisha zaidi azma ya mataifa na huifanya njia ya haki kuwa wazi zaidi. Na kadiri shahada hii inavyokuwa ya hadhi ya juu zaidi, ndivyo baraka zake kwa Umma wa Kiislamu zinavyozidi kuongezeka na kuwasha zaidi nuru ya harakati yake.

Ujumbe wa pili ni kushindwa kwa hesabu na mipango ya mfumo wa ubeberu:

Katika vita hivi vya tatu vya kulazimishwa, adui msaliti na mhalifu alikuwa ameweka matumaini ya kufanikisha malengo ambayo yalibakia kuwa ndoto za mchana zisizotimia, na kwa mara nyingine kichwa chake kikagonga mwamba. Mpango wa kuivunja Iran vipandevipande, kuuangusha mfumo wa utawala, kulazimisha taifa la Iran kujisalimisha, kutawala utajiri wa taifa, kuhakikisha usalama wa utawala wa Kizayuni na kuuangamiza Mhimili wa Muqawama, umefutika kwa baraka za damu ya Imam, makamanda, mashahidi wa Minab na maelfu ya mashahidi waliovikwa sanda za damu wa taifa la Imam Hussein nchini Iran.

Adui hakufikia hata moja ya malengo hayo; bali alipata pigo kubwa. Kuelezea kwa undani namna heshima na nguvu ya dola kubwa zaidi duniani ilivyovunjika kunahitaji miaka mingi ya tafiti za kina. Kuharibiwa kwa kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hili, kuangamizwa kwa malengo ya kimkakati ya Israel, kuongezeka kwa nguvu za Muqawama, kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, kufufuka na kuimarika kwa umoja wa taifa la Iran, kubatilika kwa mradi wa kuienezea Iran hofu duniani, kuongezeka kwa uungwaji mkono wa Iran kutoka kwa mataifa mbalimbali, kufichuliwa kwa sura mbaya ya Marekani na Wazayuni wauaji wa watoto, pamoja na kujitokeza kwa Iran kama dola kubwa yenye nguvu, ni miongoni mwa mihimili muhimu ya ushindi wetu mkubwa katika vita hivi.

﴿إِنْ تَنْصُرُوا اللَّهَ یَنْصُرْکُمْ وَیُثَبِّتْ أَقْدَامَکُمْ﴾

Ujumbe wa tatu ni kuonesha umoja wa Umma:

Leo umeundwa mstari mmoja wa umoja unaojumuisha Hizbullah ya Lebanon, Ansarullah ya Yemen, Hashd al-Shaabi ya Iraq na Muqawama wa Palestina, ambao unapaswa kuendelea kuimarika na kuungana zaidi kila siku. Katika zama za fitna zilizojaa utata, hakuna mtaji wenye thamani zaidi kwa Umma wa Kiislamu kuliko mshikamano, utambuzi sahihi na kuwajibika.

Ni lazima itambuliwe kwamba kipindi hiki ni wakati wa maamuzi makubwa na wa kuamua hatima. Enzi mpya ya nguvu ya Iran, Uislamu na Mhimili wa Muqawama imeanza. Mabadiliko haya makubwa ni matunda ya karne nyingi za juhudi na mapambano ya wanazuoni wa Mwenyezi Mungu na mataifa yenye utambuzi, yaliyoanza na Imam Mkuu, Imam Khomeini (Qudisa Sirruh), na kuendelezwa na Imam Shahidi (ra). Huu ni urithi uliokomaa kwa ajili ya kuukomboa Umma na waliodhulumiwa kutokana na mateso ya karne nyingi, kwa ajili ya kuibuka kwa mihimili mipya ya nguvu na ustaarabu mpya wa Kiislamu, na kuandaa mazingira ya kudhihiri kwa Jua Kuu la Wilaya. Kuuelewa kwa usahihi mlinganyo na mabadiliko ya kipindi hiki ni wajibu ulio juu ya mabega ya wote wanaoujali Umma na wanafikra wake.

Sherehe ya mazishi ya mwili huu mtukufu inapaswa kurekodiwa kama tukio la kipekee lisilofungwa na mipaka ya wakati wala mahali. Mkusanyiko wa shakhsia kubwa za ulimwengu wa Kiislamu, alama za kimataifa, vyombo vya habari vyenye ushawishi vya Umma wa Kiislamu, wanazuoni, wasomi, wapiganiaji na watu huru duniani vitasaidia kuifanya hamasa hii ing'ae katika kiwango cha kimataifa na kufikisha ujumbe mkubwa wa Imam Shahidi kwenye nyoyo za watu katika mabara yote, hususan katika ulimwengu wa Kiislamu. Ushiriki huu mkubwa utakuwa wenyewe ni sauti kubwa ya kuthibitisha uhalali wa njia hii na kuhuisha ahadi kwa mfumo wa imani, uadilifu, uhuru, heshima, Muqawama na matumaini ya siku zijazo. Mazishi haya yataandika ukurasa wa dhahabu katika historia ya nchi hii na ya ulimwengu wa Kiislamu.

Ninawaalika wananchi wa matabaka yote, wapenzi wa shule ya fikra ya Imam Khomeini na Imam Khamenei, pamoja na wote walioguswa na msiba huu mkubwa, washiriki kwa wingi katika tukio hili adhimu ili waoneshe nafasi ya kipenzi huyo katika nyoyo za watu watukufu, na watume ujumbe kwamba njia ya Mapinduzi na ya shahidi huyo wa Ramadhani itaendelea, na kwamba kisasi cha damu ya wananchi watukufu na mashahidi wenye hadhi kitachukuliwa.

Katika wakati huu, inawezekanaje kutomkumbuka mjenzi wa harakati hii kubwa, Imam Khomeini (ra); mhuishaji ambaye kwa fikra zake za juu aliweka msingi wa Mhimili wa Muqawama na akaianzisha safari ya msafara wa mashahidi. Imam Shahidi alikuwa mwendelezaji wa kweli wa njia hiyo na shule hiyo ya fikra, na alisimama imara katika njia ya malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu hadi pumzi yake ya mwisho, akajitoa mhanga kwa ajili ya wananchi na Iran ya Kiislamu.

Leo jukumu limeongezeka maradufu juu ya Hawza za Kielimu, vyuo vikuu, wasomi, wanafikra na wanahabari. Ni lazima ushiriki huu ugeuzwe kuwa harakati ya kudumu ya kiutamaduni, kielimu na kiustaarabu. Wajibu wetu ni kubainisha ukweli, kuhifadhi urithi wa fikra, kuchora upeo wa siku zijazo na kuendeleza njia hii. Watu wakubwa katika historia ya Uislamu hugeuka kuwa shule za kudumu ambazo vizazi vinavyofuata hupata msukumo kutoka kwake.

Kuendeleza njia ya Imam Shahidi kunapatikana kupitia ufuasi wa kweli wa utambuzi na wa kiimani kwa Waliyyul Faqih wa zama hizi. Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hadhrat Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei, ndiye mwendelezo ulio wazi na wenye nuru wa uwepo, fikra na mfano wa uongozi uliobarikiwa wa Imam Shahidi huyo.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ainue daraja shahidi huyu mpendwa na amuunganishe na Mawalii Wake, awape Umma subira na utambuzi, auimarishe umoja wa Umma wa Kiislamu, aupe nguvu mhimili wa Muqawama, ayaamshe mataifa na aweke mazingira ya kutimia kwa ahadi za Mwenyezi Mungu.

Njia iko wazi, na msafara unaendelea kusonga mbele.

﴿وَاللَّهُ غَالِبٌ عَلَىٰ أَمْرِهِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴾

Na amani iwe juu ya waja wema wa Mwenyezi Mungu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha